Rais William Ruto amesema Kenya imejitolea kuimarisha ushirikiano na Slovenia, ili kufanikisha Maendeleo endelevu, Amani, na Ustawi, kwa manufaa ya raia wa nchi hizo mbili na ulimwengu kwa jumla.
Akizungumza kwenye mkutano wa pamoja wa wanahabari na Rais wa Slovenia Nataša Pirc Musar, kiongozi wa taifa alithibitisha kuwa nchi hizo mbili zitaimarisha biashara na uwekezaji, huku zikishirikiana kutumia vilivyo manufaa ya makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Kenya na Umoja wa Ulaya, ambayo yatasaidia kuchochea ukuaji wa chumi za nchi hizo mbili.
Rais Ruto alisema kuwa walitia saini Mkataba wa Maelewano kuhusu mashauriano ya kisiasa ambayo yatapiga jeki ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Kwa upande wake Rais Musar alisema Slovenia na Kenya zitashirikiana katika vita dhidi ya ugaidi duniani na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Rais Musar anayefanya ziara rasmi ya siku tatu humu nchini ataungana na Rais Ruto kuadhimisha sherehe za 62 za sikukuu ya Madaraka Jumapili katika kaunti ya Homa Bay.
Hii ndio ziara ya kwanza kufanywa na Rais wa Slovenia hapa nchini.