Kenya imejitolea kuimarisha uhusiano wake na Muungano wa Milki za Kiarabu (UAE), ili kuboresha biashara, uwekezaji na makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi (CEPA).
Aidha uhusiano huo unakusudiwa kufanikisha upatikanaji wa fursa za ukuaji, nafasi za ajira na ustawi wa pamoja.
Hayo yalisemwa na Rais William Ruto, alipokutana na ujumbe kutoka UAE ulioongozwa na mwenyekiti wa chama cha biashara na viwanda, kujadili mbinu za kupanua biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
“Mazungumzo yetu yalilenga kuimarisha ushirikiano katika miundo mbinu na nishati, ikiwa ni pamoja na kuwezesha sekta ya nishati ya Kenya kuzalisha megawati 10,000 za nishati katika muda wa miaka saba ijayo, ujenzi wa safu mbili za kilomita 10,000 za barabara, kupanua bandari na ujenzi wa mabwawa 50 makubwa kupitia ushirikiano wa serikali na sekta ya umma ili kupiga jeki unyunyizaji maji mashamba na utoshelevu wa chakula,” alisema kiongozi wa taifa.
Kulingana na Rais Ruto, nchi hizo mbili zinaimarisha ushirikiano katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na ile ya ubunifu na kuwasawazisha vijana wa kenya ambao wanaendeleza mabadiliko ya kidijitali.
Mkutano huo, uliandaliwa katika Ikulu ya Nairobi.