KEG, MCK zasaini MoU kutetea uhuru wa vyombo vya habari

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais wa KEG Zubeida Kananu akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MCK David Omwoyo.

Chama cha Wahariri nchini Kenya (KEG) na Baraza la Vyombo vya Habari (MCK) zimesaini Mkataba wa Maelewano (MoU) unaolenga kupigania uhuru wa vyombo vya habari, kuimarisha uanataaluma na kulinda uhuru wa uhariri kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. 

Hafla ya utiaji saini mkataba huo, iliyofanyika leo Alhamisi, ilihudhuriwa na Rais wa KEG Zubeida Kananu na Mkurugenzi Mtendaji wa MCK David Omwoyo na kushuhudiwa na maafisa wengine wa taasisi hizo mbili.

Kananu ameshabikia hatua hiyo akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi pamoja kuhakikisha sekta ya vyombo vya habari inafanikiwa katika utendaji kazi wake.

“Hatuwezi tukafanya kazi kwa kujitenga. Huku wanahabari wengi vijana wakijiunga na taaluma hii, ni muhimu kuwaandaa ipasavyo kwa ajili ya kufanya kazi katika vyumba vya habari,” alisema Kananu wakati wa hafla hiyo.

Kauli zilizounga mkono na Omwoyo aliyetoa wito wa umma kupewa kipaumbele na vyombo vya habari katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Pamoja, tunaweza tukajenga vyombo vya habari zinavyowajibika zaidi ambayo kwa kweli vinahudumia umma,” alisema Omwoyo.

Taasisi hizo mbili zimekuwa mstari wa mbele kulaani ukandamizaji wa vyombo vya habari hususan wakati wa maandamano yaliyoshuhudiwa nchini miezi michache iliyopita ambapo wanahabari kadhaa walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo.

Zimetaka wanahabari kupewa fursa ya kumulika maovu katika jamii pasi ya kuandamwa na vikwazo vya aina yoyote.

 

Share This Article