Kaunti ya Kwale yapokea vifaa vya hospitali kutoka kwa wafadhili

Tom Mathinji
1 Min Read
Gavana wa Kwale Fatuma Achani apokea vifaa vya matibabu kutoka shirika la kijamii la Annick.

Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani, amepokea vifaa vya hospitali kutoka kwa shirika la kijamii la Annick, ili kufanikisha utoaji huduma bora za afya.

Vifaa hivyo vilivyotolewa na shirika hilo, vinajumuisha vitanda sita vya kisasa, viti 11 vya magurudumu na vifaa 5 vya kuwasaidia wagonjwa  kutembea.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kwale , iliyo kaunti ndogo ya Matuga, Gavana Achani alipongeza ushirikiano huo akiutaja utawafaidi pakubwa wagonjwa kwenye eneo hilo.

“Tunafuraha kwa msaada wa vifaa hivi. Vitanda hivyo na vifaa vya kuwasaidia wagonjwa kutembea, vitawapunguzia mzigo  wahudumu wetu wa afya kuwashughulikia wagonjwa, hususan katika vitengo vya dharura,” alisema Achani.

Matamshi ya Achani yaliungwa mkono na Naibu Gavana wa Kwale Josephat Chirema Kombo, aliyerejelea kujitolea kwa kaunti ya Kwale kuhakikisha utoaji huduma za afya za ubora wa hali ya juu.

Mpango huo ulioongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Annick Eddy Van Uytsel, ni sehemu ya juhudi za shirika hilo kuunga mkono miradi ya Afya, Elimu na upatikanaji wa maji katika kaunti ya Kwale.

Share This Article