Mwigizaji wa Uingereza Kate Winslet ana wasiwasi kuhusu matumizi kupita kiasi ya upasuaji wa urembo na dawa za kupunguza uzito hali inayozidi kuongezeka kote ulimwenguni.
Winslet aliyeigiza kama Rose DeWitt Bukater, kwenye filamu ya mwaka 1997 ya Titanic, anadai kwamba baadhi ya watu hawatumii mambo haya ili kuwa bora bali wanayatumia ili kuwa mtu mwingine.
Akizungumza kwenye mahojiano, Kate aliangazia sababu zake za kutotekeleza taratibu zozote za urembo awali, akisisitiza kwamba hajawahi kufanyiwa upasuaji wowote.
Anasema inamuumiza sana kuona wanawake fulani ambao tayari ni warembo wakifanya marekebisho na kuongeza sehemu fulani za mwili huku wakipunguza nyingine, jambo analosema ni la kutisha kuona mtu akiunganisha thamani yake binafsi na mwonekano wake.
Kate anasema wakati mwingine ni jambo la kuchanganya kwani wengine tayari ni wazuri katika hali zao asilia lakini bado anachukua hatua ya kufanya mabadiliko.
Alishangaa iwapo wanaopendelea vitu hivyo, wanajua wanachojiingizia ndani ya miili yao akiongeza kwamba hawajali afya zao wenyewe na hilo linatisha hata zaidi.
Haelewi jinsi mtu anaamua kuweka akiba ya pesa nyingi ili tu aweze kugharamia upasuaji wa kuongeza urembo.
Kate Winslet alimalizia kushauri watu maarufu na hata wanaochipuka wakome kutumia mambo hayo kwani mashara yake huenda yakawa makubwa.