Matamshi ya juzi Jumapili ya kiongozi wa kanisa la AIC Kenya Kasisi Abraham Mulwa kwamba atawalaani viongozi wa eneo la Ukambani wataopinga ziara ya Rais William Ruto katika eneo hilo yanaendelea kuibua hisia mseto kutoka kwa baadhi ya viongozi.
Akizungumza mjini Machakos, mwenyekiti wa chama cha KANU tawi la Machakos Peter Thuva amemtaka Kasisi Mulwa kuwaomba Wakristo mshamaha kutokana na matamshi yake kwamba atawalaani viongozi wa eneo la Ukambani.
Ameyataja matamshi hayo kama yasiyo na msingi wa dini ya Kikristo na ya kupotosha wapiga kura ambao wana uhuru wa kuchagua viongozi wanaowataka wao wenyewe.
Aidha, ametoa wito kwa maelfu ya vijana waliojiandikisha kupata vitambulisho kufika katika afisi za Chifu na Huduma Centre mjini Machakos kuchukua vitambulisho vyao kwa ajili ya kujiandikisha kama wapiga kura kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 na chaguzi ndogo katika wadi ya Muumbuni ambapo mwakilishi wadi alifariki miaka miwili iliyopita.
Jumapili iliyopita, Kasisi Mulwa alitoa tamko la kuwalaani wanasiaaa kutoka eneo la Ukambani ambao watajaribu kupinga ziara ya Rais Ruto eno hilo na kusema kwamba laana hiyo itawanyima nafasi ya kuchaguliwa tena mwaka 2027.