Afisi ya mwanasheria mkuu imetangaza kwamba kamati itabuniwa ya kufanikisha mabadiliko katika sekta ya elimu ya kisheria nchini, baada ya kuandaa mkutano wa majadiliano na washikadau wa sekta ya sheria nchini.
Kamati hiyo itakuwa chini ya uenyekiti wa mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya sheria nchini almaarufu Kenya Law Reforms na itapatiwa muda wa miezi miwili kuibuka na ripoti kuhusu mabadiliko yanayohitajika.
Hatua ya mwanasheria mkuu na idara ya ya sheria nchini inafuatia malalamishi ambayo yamekuwa yakiibuliwa katika sekta ya elimu ya sheria nchini kama vile mtindo wa usajili wa wanafunzi wanaosomea kozi za kisheria na uwazi wa mchakato mzima wa mtihani.
Mengine yanajumuisha ufadhili wa taasisi za elimu ya kisheria nchini, kiwango cha karo kwa wanaosomea uanasheria nchini na usaidizi kwa wanafunzi wanaotaka kusomea kozi hizo lakini hawana uwezo wa kifedha.
Kamati itakayobuniwa inatarajiwa kukusanya malalamishi ya wanafunzi na wadau wengine wa sekta hiyo na athari za maagizo ya mahakama kuhusu masuala kama hayo.
Itatumia mbinu mbali mbali ikiwemo kukutana na walalamishi na kuwasikiliza moja kwa moja pamoja na mapendekezo ya kuboresha sekta ya elimu ya kisheria nchini.
Waliohudhuria mkutano wa leo ni mwanasheria mkuu, rais wa chama cha wanasheria nchini LSK, wenyeviti wa taasisi ya Kenya School of Law, wawakilishi wa baraza la elimu ya kisheria nchini na wawakilishi wa tume ya mabadiliko ya kisheria nchini.