Kalonzo: Raila ndiye mfungwa wa kisiasa aliyeteseka sana nchini

Marion Bosire
2 Min Read

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, amesema kwamba marehemu Raila Odinga ndiye mfungwa wa kisiasa aliyeteseka muda mrefu zaidi nchini Kenya.

Musyoka alisema hayo katika ujumbe wake wa kumwomboleza Rais ambapo alisema kwamba wakati wa kupigania demokrasia ya vyama vingi, mwili wa Raila ulipata majeraha ya mishale, risasi na hata rungu, uchungu ambao anahisi hakuna yeyote angevumilia.

“Hata hivyo kila baada ya kuachiliwa, angeinua mkono wake juu akiwa amekunja ngumi kwa kujitolea akiamini kwamba uchungu aliopitia ungezaa demokrasia na uhuru wa taifa pendwa la Kenya,” aliandika Kalonzo.

Kiongozi huyo wa Wiper ambaye alimuunga mkono Raila Odinga katika kuwania Urais mara kadhaa alisema hiyo ndiyo sababu huwa wanamrejelea Raila kama bingwa wa ukombozi wa pili wa kisiasa nchini Kenya.

Kalonzo katika ujumbe wake alielezea jinsi alipokea habari za kifo cha Raila punde baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Heathrow jijini London, nchini Uingereza ambako anapangiwa kuwa kwa muda wa siku 10.

Alisema kwamba kwa muda ambao amehusiana na Raila katika siasa, alielewa fika ni kwa nini alipatiwa majina mazuri likiwemo Baba.

“Kutoka upinzani hadi upande wa serikali kama waziri mkuu, hadi Agosti 27, 2010 katiba yetu mpya ilipozinduliwa rasmi, ndugu yangu Raila alitekeleza jukumu muhimu.” aliandika Kalonzo.

Raila Odinga alikata roho leo asubuhi nchini India ambako alikuwa akipokea matibabu.

Share This Article