Kaka ya mwanamuziki 2Face Idibia au 2Baba aitwaye Charles, amefichua mengi kuhusu uhusiano wa kimapenzi kati ya mwanamuziki huyo na mwanamke kwa jina Natasha.
Charles ambaye ni mdogo wa 2Baba ametumia akaunti yake ya Instagram kumlilia kakake akidai kwamba ametekwa na Natasha kiasi kwamba anajisahau.
Huku akimtaja kuwa mpole na mwenye moyo safi mithili ya Yesu Kristo, Charles amemtaka kakake aamke kutoka usingizi ambao amelala na ajiokoe.
“Sio hatia kujiokoa na kuendelea kutoka mahali ambapo ulikaribia kupoteza maisha yako, lakini haujasonga mbele, umetekwa,” aliandika Charles akiongeza kwamba mwanamuziki huyo aliacha uhusiano mbaya na aliyekuwa mke wake Annie lakini sasa ameingia kwenye balaa kubwa zaidi.
Charles alifichua kwamba Natasha alitumia simu ya 2Face kutangaza talaka yake na Annie Macauley, huwa anachapisha picha zake na kufuta kwenye akaunti ya mwanamuziki huyo huku akiomba wafuasi wake wamlazimishe amuoe.
Natasha anadaiwa pia kudukua mtandao wa Whatsapp wa mwanamuziki huyo ambapo alifuta jumbe ambazo hazikumfurahisha na kujibu nyingine bila idhini.
“Amekushawishi uachane na usimamizi wako na kutelekeza biashara zako jijini Lagos na kuhamia Abuja,” aliendelea kulalamika Charles akisema huko Abuja, kakake amefanywa msaidizi bila kupenda na huwa anapelekwa kila mahali hadi Benin, maeneo ambayo kwa kawaida hawezi kuzuru.
Lalama za Charles zinajiri baada ya 2Baba kuomba msamaha kuhusiana na aliyoyasema katika mahojiano ambapo alikosa kumtaja Natasha na kulingana na Charles, Natasha ndiye amemlazimisha mwanamuziki huyo aombe msamaha.
Bila kutaja kosa alilofanya katika mahojiano hayo na Nedu, 2Face alimrejelea Natasha kama mke wake na kummiminia sifa kabla ya kuomba msamaha.