Wizara ya Kilimo na Ustawi wa Mifugo, imelaani uharibifu na wizi katika ghala la Halmashauri ya Nafaka na Mazao Nchini(NCPB) tawi la Maua, kaunti ya Meru siku ya Jumatano Juni 25,2025 wakati wa maandamanao ya Gen Z.
Kupitia kwa taarifa, waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe, alitaja shambulizi hilo katika maghala ya NCPB kuwa dhuluma kwa utoshelevu wa chakula hapa nchini.
“Shambulizi hilo kwenye ghala la NCPB sio tu uhalifu, lakini dhuluma dhidi ya utoshelevu wa chakula hapa nchini,” alisema Kagwe.
Waziri huyo aliongeza kuwa: “Mbolea iliibwa, ambayo ilikusudiwa kuwasaidia wakulima wakati wa msimu wa upanzi. Uhalifu huo umehujumu uwezo wa wakulima kuzalisha chakula, kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa familia zao na kupiga jeki uchumi wa taifa.”
Uchunguzi wa awali umebainisha kuwa zaidi ya magunia 7,354 ya mbolea kila moja ikiwa na uzani wa kilo 50 yote ya thamani ya shilingi milioni 29.5, yaliibwa kutoka kwa ghala hilo.
“Wale ambao wanaiba na kuharibu miundomsingi ya umma, sio waandamanaji ila ni wahalifu na wanapaswa kuchukuliwa hatua,” alidokeza Kagwe.
Alitoa wito kwa Huduma ya Taifa ya Polisi kuharakisha kuwatia nguvuni wale walioharibu na kuiba mbolea hiyo.