Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Mutahi Kagwe amewaonya wanasiasa dhidi ya kutumia bei za majani chai kuwa mashindano ya kisiasa ya kikanda.
Waziri alisema changamoto zinazoathiri sekta ya chai ni za kiufundi na zinapaswa kushughulikiwa kupitia uingiliaji kati wa sera, uboreshaji wa viwango vya ubora, na data ya soko na sio matamshi ya kisiasa.
Akizungumza katika eneo la Kanja, kaunti ya Embu, wakati wa uzinduzi wa mashini 13 za kisasa za kuhifadhi maziwa zenye thamani ya shilingi milioni 77.9, Kagwe alisema vituo hivyo vitahudumia zaidi ya wakulima 3,900 na kukusanya hadi lita 25,000 kila siku.
“Wanunuzi hawalazimishwi kununua majani chai kutoka sehemu fulani. Ni chaguo lao. Wao huamua aina ya ubora wa majani chai wanaotaka,” alisema Kagwe.
Aidha, aliongeza kuwa,” Ladha ya chai sio swala la kisiasa. Ni swala la kiufundi.”
Waziri huyo alishikilia kuwa soko la majani chai linasalia wazi chini ya Halmashauri ya Maendeleo ya Majani Chai nchini (KTDA), na hakuna mkulima analazimishwa kutumia mfumo mmoja.
“Ikiwa utahisi bei sio sawa, unaweza uza moja kwa moja. Una uhuru wa kuchaguza kule utauza Majani Chai. Jukumu langu ni kuhakikisha ubora wa Majani Chai unaimarika katika maeneo yote…..tusiingize siasa kwa bei ya majani chai,” alisihi Kagwe.
Alitoa wito kwa viongozi kuepuka matamshi yanayosababisha migawanyiko, yanayoweza kudhoofisha sekta hiyo ambayo kwa muda mrefu imekuwa mojawepo ya nguzo muhimu ya kiuchumi hapa nchini.
“Hatutaki kugawanya sekta hii. Tafadhali wanasiasa msiwagawanye wananchi kwa misingi ya Majani Chai. Hakuna migawanyiko. Lengo letu ni kuhakikisha ubora wa hali ya juu wa Majani Chai na kusaidia maeneo yanayokuza zao hilo kufikia viwango hivyo,” aliongeza Kagwe.
Alielezea kujitolea kwa serikali kulinda sekta zote ndogo huku akiwataka viongozi kujifahamisha maswala ya kiufundi kabla ya kutoa matamshi yoyote.