Kabogo: Serikali imejitolea kulinda data ya kibinafsi

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali, William Kabogo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali William Kabogo amehakikishia umma kwamba serikali italinda data ya kibinafsi, itaimarisha miundombinu ya dijitali na kuboresha uvumbuzi.

Kabogo aliyasema hayo jana Jumanne katika kaunti ya Eldoret wakati wa kongamano la kila mwaka kuhusu data ya kibinafsi la mwaka 2025.

Waziri huyo alidokeza kuwa ulinzi wa data ya kibinafsi sio tu jukumu la udhibiti, bali pia kunachangia katika mageuzi ya kidijitali, pamoja na ukuaji wa kiuchumi.

Katika kongamano hilo, Kabogo alisema serikali haina nia ya kufunga majukwaa ya mitandao ya kijamii hapa nchini.

Kauli hiyo ilijiri huku kukiwa na mijadala kuhusiana na mchango wa mitandao ya kijamii katika kusambaza habari potovu, pamoja na athari zake kwa usalama wa taifa.

Kamishna wa data Immaculate Kassait, maafisa wakuu serikalini pamoja na washirika wengine walikariri uwajibikaji wao katika kuhakikisha ustawi wa uchumi wa kidijitali ulio salama na wenye ufanisi kwa raia wote.

Share This Article