Timu ya taifa ya Kenya kwa wasichana walio chini ya umri wa miaka 17, Junior Starets, iliwasili jijini Kampala, Uganda, jana jioni kwa mkondo wa kwanza wa mechi ya raundi ya pili, kufuzu kwa kombe la dunia dhidi ya wenyeji.
Mchuano huo wa kufuzu kwa kombe la dunia litakaloandaliwa mwishoni mwa mwaka huu nchini Morocco, utasakatwa Jumamosi hii katika uga wa Nakivubo jijini Kampala kuanzia saa kumi alasiri.
Kikosi hicho cha kocha Mildred Cheche kinawajumuisha wachezaji wenye tajriba na malimbukeni.
Baadhi ya wachezaji ambao walicheza mechi zilizopita za kufuzu ni pamoja na nahodha Halima Imbachi,Halima Imbachi, Mitshel Waithera, Lorine Ilavonga, Jenevive Mithel, Elizabeth Ochaka, Joy Angela Valencia, Joan Ogola, na Lindy Weey.
Kenya inalenga kufuzu kwa fainali za kombe la dunia kwa mara ya pili baada ya kufuzu kwa mara ya kwanza mwaka uliopita katika Jamhuri ya Dominika.
Mkondo wa pili utaandaliwa Nairobi tarehe 16 mwezi huu.
Mabanati wa Kenya waliondoka nchini jana jioni.