Juma Jux amwandalia mkewe hafla ya pili ya ndoa

Jux alimchumbia Priscilla Ojo kwa mara ya pili mbele ya watu wa familia yake na marafiki.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Juma Jux alimwandalia mkewe Priscilla Ojo hafla ya pili ya kufunga ndoa nchini Tanzania jana usiku.

Jux alichapisha video fupi ya hafla hiyo kwenye akaunti yake ya Instagram ambapo alifafanua kwamba alimchumbia kwa mara ya pili na zamu hii ni mbele ya familia yake na marafiki.

Jingine alilofichua mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni Juma Mussa Mkambala ni kwamba pete hiyo ya pili inazidi ile ya kwanza kwa ukubwa.

“Ninakupenda na kila kitu kilicho ndani yangu na ninasubiri kwa hamu kuwa nawe milele mpenzi wangu.” aliandika Jux.

Mama Priscilla ambaye ni mwigizaji maarufu wa Nollywood nchini Nigeria Iyabo Ojo alichapisha video za hafla hiyo huku akishukuru Mungu kwa baraka ya wanandoa hao wawili.

Jux na Priscilla walifunga ndoa mara ya kwanza kulingana na kanuni za dini ya kiisilamu Ijumaa ya tarehe 7 mwezi Februari mwaka huu wa 2025.

Iyabo alifichua wakati huo kwamba hafla moja ilikuwa imekamilika na kwamba walikuwa wanasubiri nyingine tano za ndoa ya Jux na Priscilla.

Mwigizaji wa Nollywood Toyin Abraham ambaye ni rafiki ya mama mkwe wa Jux alihudhuria hafla ya jana ambapo anaonekana kwenye video akiombea wanandoa hao kwa lugha asilia ya Yoruba.

Inasubiriwa kuona iwapo kuna hafla ambazo zitaandaliwa nchini Nigeria alikozaliwa Priscilla.

Share This Article