JSC yaanzisha uchunguzi kuhusu madai ya Jaji kupokea hongo

Marion Bosire
2 Min Read
Winfrida Mokaya, Katibu JSC

Tume ya Huduma za Mahakama nchini, JSC imesema kwamba inachunguza madai ya Jaji mmoja kupokea hongo kulingana na taarifa ambazo zimekuwa zikisambaa mitandaoni.

Katika taarifa iliyotiwa saini na Msajili Mkuu wa Mahakama Winfrida Mokaya, tume hiyo ilielezea kwamba imetambua taarifa hizo na imeanzisha uchunguzi kulingana na mamlaka iliyotunukiwa na katiba.

“Kulingana na kifungu nambari 172 na 168 cha Katiba, Tume ya Huduma za Mahakama imepatiwa mamlaka ya kukuza na kulinda uhuru na uwajibikaji wa Idara ya Mahakama”, alisema Mokaya katika taarifa yake.

Amesema kmkutokana na hilo, JSC imeanzisha uchunguzi kuhusu suala hilo huku ikithibitisha tena dhamira yake thabiti ya kuendeleza uadilifu na kuhakikisha uwajibikaji ndani ya Idara ya Mahakama.

Jana Jumapili, mitandao ya kijamii nchini Kenya ilishika moto kufuatia madai ya aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria nchini, LSK, Nelson Havi.

Havi alimzomea hadharani Jaji mmoja ambaye analaumiwa kwa kupokea hongo ya mamilioni ya pesa. Alitaja kisa kimoja ambapo Jaji huyo alidaiwa kupokea hongo ili kufutilia mbali stakabadhi muhimu kwa kesi na baadaye shahidi wa upande wa mashtaka akaomba arejeshewe pesa zake.

Leo Jumatatu, Septemba 22, 2025, Havi tena amemnyoshea kidole cha lawama Jaji wa kike ambaye anamtaja kuwa Jaji mwenye ufisadi wa kiwango cha juu nchini.

Jaji huyo, kulingana na Havi, ana hulka ya kutoa maamuzi ya moja kwa moja na baadaye kuyabadilisha baada ya kupatiwa hongo.

Share This Article