Mke wa Naibu wa Rais Dkt. Joyce Kithure, ametoa changamoto kwa wanawake barani Afrika, kupigania kusikizwa kwa sauti zao, na kutambuliwa kwa juhudi zao ili kuimarisha bara hili.
Akizungumza Ijumaa jioni wakati wa dhifa ya kwanza ya tuzo za wake wa Marais barani Afrika iliyoandaliwa jijini Nairobi, Dkt. Kithure alisema Afrika haiwezi kupuuza juhudi za wanawake, ambao wanahusika pakubwa katika maendeleo yake.
“Kote Afrika, wanawake wamekuwa nguzo muhimu katika maendeleo. Iwe ni katika biashara, Kilimo, Teknolojia au Utumishi wa Umma, wanawake wamekuza na kuimarisha mifumo ambayo inaleta pamoja jamii zetu,” alisema Dkt. Kithure.
Dkt. Kithure, ambaye ni Mwanasayansi na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alidokeza kuwa jamii ambazo zinawawezesha wanawake na wasichana hushuhudia mageuzi makubwa.
“Wakati msichana anapate elimu, rasilimali na fursa, huwa habadilishi maisha yake tu, lakini huwa anabadilisha maisha ya wale walio karibu na yeye. Yeye huwa kichocheo cha ukuaji, uvumbuzi na mageuzi ya kizazi,” aliongeza Dkt. Kithure.
Pia alitoa wito wa juhudi za kila mara za kuwawezesha wanawake na wasichana, akikariri umuhimu wa utetezi na ushirikiano baina ya wahusika wote.