John Blaq asimulia mafunzo aliyopata kwenye muziki

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda John Blaq amesimulia kuhusu mambo aliyojifunza juu ya tasnia ya muziki, akisisitiza umuhimu wa kuelewa na kuthamini mashabiki badala ya kuzongwa na viwango visivyo vya lazima.

Blaq anahisi wasanii wengi huishia kuvunjika moyo matamasha yao yanapofeli kwa sababu huwa wamejiwekea matarajio yasiyo halisi, mara nyingi wakijilinganisha na wasanii wengine wenye mashabiki wengi zaidi.

“Nimejifunza kuthamini mashabiki wangu na kutowatia presha, nikielewa kuwa nao pia wanapitia changamoto zao,” alisema.

“Kubali pale ulipo. Mradi wamekuunga mkono na maisha yako yamebadilika, usitarajie mambo makubwa kutoka kwa mashabiki. Hicho ndicho nilichojifunza.” Aliendelea kusema msanii huyo.

Blaq alieleza kuwa mashabiki, kama ilivyo kwa wasanii, hupitia changamoto mbalimbali maishani, na kwa hivyo hawapaswi kuletewa mzigo mkubwa wa matarajio ya kuhudhuria kila onyesho.

Alionya kuwa wasanii wanaoendelea kuweka matarajio ya juu kupita kiasi hujiweka katika hatari ya kuchanganyikiwa pale ambapo matarajio hayo yanakosa kutimia.

Kuhusu suala la matamasha kufeli, John Blaq anaamini tatizo lipo kwa wasanii kupuuza hali halisi ya mazingira na ushindani wao badala ya kuelekeza nguvu kwa mashabiki wao wa kweli.

“Mara nyingi tunataka kujithibitishia sisi kwa sisi na kusahau kuwa tunaimba kwa ajili ya mashabiki, si kwa kundi dogo la wasanii waliopo kwenye tasnia,” aliongeza.

“Kuna ukumbi wa kila msanii hapa Uganda — wa yule mwenye nyimbo tatu kali, kumi, au kumi na tano… lakini kila msanii anataka kukimbilia ukumbi mmoja tu ili kuonyesha kuwa anaweza kulipia, bila kufahamu kuwa hana mashabiki wa kutosha” alimalizia.

Share This Article