Mvua kubwa inatarajiwa kushuhudiwa katika maeneo mengi nchini kuanzia kesho Jumapili Machi 9 kwa kipindi cha siku tatu zijazo.
Taarifa kutoka kwa idara ya utabiri wa hali ya anga nchini imeonya kuwa mvua hiyo ya zaidi ya milimita 20, inatarajiwa kuanzia kesho katika maeneo ya Nairobi, Ziwa Victoria, bonde la Ufa, nyanda za juu magharibi mwa bonde la ufa, na nyanda za chini kusini mwa nchi.
Kiwango cha mvua hiyo kinatarajiwa kupanda hadi zaidi ya milimita 30 katika maeneo mengi nchini, kuanzia Jumatatu ijayo na kupungua kuanzia tarehe 11 mwezi huu.
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini Dkt. David Gikungu, amesema kaunti zinazotarajia mvua kubwa ni Narok, Kericho, Bomet, Homabay, Siaya, Migori, Busia, Kisumu, Kisii, Nyamira, Nandi, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Baringo, Nakuru, Trans-Nzoia, Uasin-Gishu, Elgeyo Marakwet, West-Pokot, Turkana, Marsabit, Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Nairobi, Machakos, na Kajiado.
Gikungu amewataka wananchi kuwa makini na kuchukua tahadhari kutokana na mvua hiyo kubwa itakayoandamana na ukungu na kuwataka waendeshaji magari kuwa makini.