Mwanamuziki na mwanabiashara wa Marekani Shawn Corey Carter maarufu kama Jay Z huenda amenyakua talanta chipukizi ya Nigeria Ayra Starr na kumsajili kwenye kampuni yake ya kurekodi muziki na kusimamia wanamuziki ya Roc Nation.
Jina na orodha ya kazi za binti huyo zimeangaziwa kwenye tovuti rasmi ya Roc Nation.
Haya yanajiri wiki chache baada ya kampuni hiyo ya Roc Nation kumpongeza Ayra Starr kwa kushinda tuzo yake ya kwanza ya BET na wengi wakachukulia pongezi hizo kama hatua ya kuelekea kwenye usajili.
Msanii huyo anatarajiwa kutoa wimbo wake wa kwanza chini ya kampuni ya Roc Nation uitwao “Hot Body” kulingana na tangazo kwenye akaunti yake ya Instagram na ile ya Roc Nation ya mtandao huo.
Ayra wa umri wa miaka 23 sasa bado amesajiliwa na kampuni ya Mavin Records inayomilikiwa na Michael Collins Ajereh maarufu kama Don Jazzy.
Msanii huyo wa kike mzaliwa wa Benin ambaye jina lake halisi ni Sarah Oyinkansola Aderibigbe, alianza muziki rasmi mwaka 2021 wakati alizindua EP yake ya kwanza ya “Away”.
Alijulikana mwaka 2022 alipotoa wimbo wake uitwao “Rush” ambao ulipendwa sana ndani na nje ya Nigeria na ulimfanya ateuliwe kuwania tuzo za Grammy awamu ya 66, katika kitengo cha tumbuizo bora la muziki wa Afrika yaani Best African Music Performance.