Janie Namukasa amwomba msamaha Chameleone

Mtangazaji huyo alikuwa amedai kwamba Chameleone alikamatwa na maafisa wa polisi nchini Marekani.

Marion Bosire
2 Min Read

Mtangazaji wa Uganda Janie Namukasa amemwomba msanii nguli wa muziki wa taifa hilo Jose Chameleone msamaha baada ya kutoa habari za uongo kumhusu.

Katika video aliyochapisha mitandaoni februari 23, 2025, Namukasa alikiri kwamba habari alizotoa awali juu ya Jose Chameleone ni za uongo.

Alisema alipatiwa taarifa hizo na watu fulani lakini baadaye aligundua kwamba hazikuwa za ukweli na kwamba watu hao walikuwa wakizozana na Jose Chameleone.

Namukasa alimtakia Chameleone anayeugua ugonjwa wa kongosho afueni ya haraka huku akimwomba amsamehe kwa kuumiza hisia zake.

Mtangazaji huyo wa kituo cha redio cha Radio 4 ambaye pia huchapisha taarifa za burudani kwenye mitandao kama YouTube na TikTok, alidai awali kwamba Chameleone alikuwa amekamatwa nchini Marekani kwa kushambulia mwenyeji wake Juliet Zawedde.

Baadaye ilibainika kwamba watu walioonekana nyumbani kwa Juliet Zawedde nchini Marekani wakimchukua Jose Chameleone walikuwa wahudumu ambao walikuwa wakimpeleka hospitalini kwa upasuaji.

Chameleone alijibu madai hayo ya Namukasa kupitia video aliyorekodi akiwa kwenye kitanda cha hospitali ambapo alionya dhidi ya usambazaji wa taarifa za uongo.

Alifahamu kuhusu madai hayo ya uongo baada ya kutumiwa video na Abitex, mwandalizi wa matamasha anayefahamika sana nchini Uganda.

Wakati huo Chameleone aliyekuwa akisubiri kufanyiwa upasuaji, alihakikishia mashabiki wake kwamba angewafahamisha kuhusu hali yake ya kiafya huku akishukuru waliokuwa wakimwombea apone.

Namukasa aliomba msamaha baada ya Chameleone kutaka msamaha hadharani na fidia ya shilingi milioni 100 katika muda wa siku tano la sivyo achukue hatua za kisheria.

Share This Article