Huku taifa linapoomboleza kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, jamii ya Kalenjin inatarajiwa kuzuru familia ya marehemu Raila Odinga ili kuifariji na kuwasilisha rambirambi zao.
Ujumbe huo pia utawasilisha mafahali 80 kwa familia ya Odinga, kama ishara ya kuashiria miaka 80 aliyoishi Raila kama utambulisho wa heshima uliokita mizizi katika jamii ya Kalenjin.
Ujumbe huo ukiongozwa na mbunge wa Tinderet Julius Melly ambaye ndiye huongoza kikao cha wabunge wa jamii za Kipsigis, ulisema ziara hiyo ni sehemu ya sherehe ya kitamaduni inayonuiwa kuimarisha urafiki na heshima baina ya jamii ya Kalenjin na ile ya Waluo.
Melly alisema ishara hiyo inanuiwa kuashiria undugu, amani na mshikamano uliopo baina ya jamii hizo mbili. Aliongeza kuwa ziara ya wazee wa jamii ya Kalenjin haikuwa tu suala la kutoa rambirambi bali pia thibitisho la undugu uliokuwapo baina ya rais William Ruto na marehemu Raila Odinga, uliosaidia kuimarisha umoja baina ya jamii hizo mbili ambazo zimekuwa mahasimu tangu jadi.
Raila aliyekuwa na umri wa miaka 80, alifariki mnamo Jumatano nchini India akipokea matibabu. Rais Ruto alitangaza siku saba za maombolezo kwa ajili ya kumuenzi.