Mchekeshaji na mwigizaji wa Marekani Jamie Foxx alibubujikwa na machozi kwenye jukwaa la tuzo za BET zilizoandaliwa Jumatatu usiku kulingana na saa za Marekani.
Msanii huyo alikuwa akitoa hotuba ya kukubali tuzo aliyotunukiwa ya nyota wa kipekee alipokumbuka jinsi alijipata pabaya kiafya mwaka 2023 nusura aage dunia.
Alikubali tuzo yake aliyopokezwa na Stevie Wonder kisha akaanza kulia akisimulia alivyoponea huku akiahidi Mwenyezi Mungu
kwamba atahakikisha ametenda mema kwani alimpa fursa ya pili maishani.
Foxx alisema hatasahau mahali ambapo ametoka akishukuru wasanii wengine wamarekani weusi ambao anasema wamemsaidia sana hasa katika maandalizi na mauzo ya onyesho lake la Netflix liitwalo “Jamie Foxx: What Had Happened Was… “.
Aliwataja mabinti zake waliokuwa wakihudhuria tuzo hizo na ambao walikuwa pia wakitokwa na machozi kufuatia hotuba yake ambapo alisema kwamba mmoja wap wa umri wa miaka 14 Anelise alimchezea gitaa akiwa amelazwa hospitali.
Kulingana na Foxx, Anelise alikuwa akiingia kwenye chumba chake cha hospitali kisiri na kumchezea gitaa hatua iliyofanya hali yake iboreke.
Hakumsaaza binti yake mwingine aitwaye Corinne ambaye alisema pia kwamba usaidizi aliompa wakati alikuwa akiugua ulikuwa wa maana sana.
Jamie alikimbizwa hospitalini akiwa hali mbaya Aprili mwaka 2023 akiugua ugonjwa usiojulikana ambao baadaye ulibainika kuwa kiharusi na tatizo la kuvuja damu kwenye ubongo.
Matatizo hayo ya kiafya yalimkumba akiwa kwenye maandalizi ya filamu iitwayo “Back in Action” na Cameron Diaz kazi ambayo alimalizia baada ya kupata nafuu. Filamu hiyo ilizinduliwa Januari mwaka huu.