Jaji wa Umoja wa Mataifa ambaye ni raia wa Uganda amehukumiwa kifungo cha miaka sita na miezi minne gerezani baada ya kupatikana na kosa la kumlazimisha mwanamke kufanya kazi kama mtumwa wa nyumbani.
Lydia Mugambe mwenye umri wa miaka 50, alikuwa ni Jaji wa Mahakama Kuu nchini Uganda tangu mwaka 2013 na aliteuliwa katika Mahakama ya Umoja wa Mataifa 2023.
Hadi kukamatwa na kufungwa jela, Mugambe alikuwa akisomea Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Oxford wakati polisi walipogundua alikuwa na msichana mdogo wa raia wa Uganda nyumbani kwake akifanya kazi bila malipo kama mjakazi.
Mugambe, alihukumiwa kufungwa katika Mahakama ya Oxford siku ya Ijumaa baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya utumwa wa kisasa mwezi Machi.
Katika hukumu hiyo, Jaji David Foxton alimwambia mshtakiwa “hakuonyesha kujutia kabisa” kwa kitendo chake na alikuwa anatazamia “kumlaumu” muathiriwa kwa kile kilichotokea.