Jaji Mkuu Koome, Waziri Murkomen wafanya mashauriano

Martin Mwanje
2 Min Read
Waziri Kipchumba Murkomen akiwa na Jaji Mkuu Martha Koome
Jaji Mkuu Martha Koome leo Jumatano amekuwa mwenyeji wa Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen aliyemtembelea katika majengo ya Mahakama ya Juu jijini Nairobi.
Wakati wa mkutano kati yao, wawili hao walizungumzia njia bora za kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kuboresha usalama wa idara ya mahakama na maafisa wake.
“Pia tulijadili ushirikiano juu ya utozaji wa faini za papo hapo barabarani ili kuimarisha usalama kwenye barabara zetu na kuondoa mrundiko wa kesi katika mahakama,” alisema Murkomen baada ya mkutano wao.
Mkutano kati ya Koome na Murkomen unakuja wiki chache baada ya Jaji Mkuu huyo kuinyoshea serikali kidole cha lawama kwa kuondoa maafisa wake wa ulinzi.
Hata hivyo, Murkomen alikanusha madai ya Jaji Mkuu ya kupokonywa walinzi wake akisema maafisa walioondolewa walikusudiwa kupewa mafunzo zaidi baada ya kupandishwa vyeo.
Mwishoni mwa mwaka jana, Idara ya Mahakama iliulaumu  uongozi mkuu wa nchi kwa kuondoa walinzi wa Jaji Lawrence Mungambi ambaye alimhukumu kifungo cha miezi sita gerezani kaimu Inspekta Mkuu wa Polisi Gilbert Masengeli.
Wakati huo, Koome ambaye pia ni mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Mahakama alilaani kitendo hicho akisisitiza umuhimu wa Idara ya Mahakama kufanya kazi bila mapendeleo wala kushurutishwa.
Tangu wakati huo, uhusiano baina ya idara hiyo na uongozi mkuu wa nchi umekuwa wa vuta ni kuvute na haijabainika ikiwa mkutano wa hivi punde kati ya Jaji Koome na Waziri Murkomen utatuliza mivutano baina ya pande hizo.
Share This Article