Jaji Mkuu Martha Koome ametoa wito wa jamii yote kuhusika katika kuangamiza ajira ya watoto nchini Kenya.
Koome amesisitiza umuhimu wa taasisi zote kushirikiana kuangamiza uovu huo akisema ingawa Idara ya Mahakama hutekeleza wajibu muhimu, haiwezi ikafanikisha hilo peke yake.
Hususan, Jaji Mkuu ametoa wito kwa bunge kuimarisha na kuzifanya sheria za kuwalinda watoto kuwa za kisasa huku serikali kuu ikitakiwa kutekeleza sheria madhubuti na kutenga rasilimali za kutosha kuhakikisha hilo linatimia.
Aidha, ameitaka sekta binafsi kukumbatia mienendo ya kibiashara inayozingatia maadili nayo mashirika ya kijamii na jamii kwa jumla kupigania haki za watoto na kuwalinda katika ngazi ya vijijini.
Kulingana naye, kila taasisi na raia wana wajibu muhimu wa kutekeleza katika kuangamiza ajira ya watoto nchini.
“Kongamano hili linatoa fursa muhimu ya kukuza wajibu wa pamoja. Kwa kuakisi pamoja, kubadilishana tajiriba na kutafuta suluhu pamoja, tunakaribia kujenga Kenya ambako hakuna mtoto anayetumiwa vibaya,” alisema Koome wakati akifungua Kongamano la Kila Mwaka la Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi (ELRASE III).
“Haki kwa watoto ni haki kwa jamii. Katika kulinda haki zao, tunalinda watoto wetu, tunalinda mustakabali wetu. Kwa kuwapa elimu na uhuru wa kutofanya kazi, tunalipa taifa letu viongozi wapya, wabunifu, na watu wenye maono. Kwa kuangamiza ajira ya watoto, tunaheshimu siyo tu majukumu yetu ya kikatiba bali pia wajibu wetu wa kimaadili kama binadamu.

Maudhui ya kongamano hilo ni “Uangamizaji wa Aina Zote za Ajira ya Watoto na Upatikanaji wa Haki.
