Mwanasiasa maarufu wa Uganda Dkt. Kizza Besigye amefikishwa katika Mahakama Kuu mjini Kampala kusikiliza ombi la mawakili wake la kumtaka achiliwe huru.
Besigye, ambaye amesusia chakula tangu wiki iliyopita, alionekana kudhoofika huku akiandamana na mshtakiwa mwenzake Haji Obeid Lutale.
Awali, Jaji wa Mahakama Kuu aliaamrisha waandishi wa habari kuondoka nje ya kikao cha mahakama na baada ya kufanya mkutano wa faragha na upande unaomtetea Besigye, waandishi hao wa habari walirejea kwenye kikao hicho.
Douglas Singiza, Jaji wa Mahakam Kuu ya Uganda ameagiza maafisa wa gereza kuwarejesha Besigye na Lutale gerezani kutokana na kudhoofika kwa afya yake.
Kikao cha mahakama kiliendelea bila wawili hao. Mawakili wanaitaka Besigye aachiliwa kwa misingi ya matibabu.
Jaji huyo ameagiza Besigye na mshtakiwa mwenzake kurejeshwa gerezani.
Jana Jumanne, Waziri wa Sheria na Masuala ya Kikatiba Nobert Mao aliliambia bunge kuwa Mahakama Kuu ya Uganda itaanza mchakato wa kusikiliza ombi la mawakili wa mwanasiasa huyo ungeanza leo, badala ya Jumanne ya wiki ijayo kama ilivyokuwa imepangawa awali.
Wakili wa Besigye Eron Kiiza ambaye awali alihstakiwa na kuhukumiwa miezi tisa jela na mahakama ya kijeshi, pia amefikishwa mahakamani.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni kupitia mtandao wake wa X jana alishtumu Mahakama ya Juu nchini humo kwa kuchelewesha mchakato wa kesi ya mwanasiasa huyo wa upinzani ilipotoa uamuzi wa kuivua mamlaka ya kisheria Mahakama ya Kijeshi kusikiliza kesi za raia wa kawaida.