Mwanamuziki wa Marekani Ja Rule amesema mwanamuziki mwenza Fat Joe yuko sawa hata anapokabiliwa kisheria na madai ya kushiriki ngono na mtoto.
Msanii huyo wa mtindo wa Rap wa muda mrefu alikuwa akizungumza na wanahabari pembezoni mwa tamasha la Summer Jam huko New Jersey nchini Marekani Ijumaa.
Wanahabari hao ndio walimtupia maswali ya kutaka kufahamu hali ya rafiki yake ambapo alielezea kwamba yuko sawa na wanawasiliana mara kwa mara.
Alifichua kwamba walizungumza kwa simu na mwanamuziki huyo ambaye kando na kuwa rafiki yake ni mzaliwa mwenza wa New York, kabla yake kuingia jukwaani katika tamasha hilo.
Ja Rule alitaka kujua iwapo Joe angejiunga naye jukwaani lakini akapata kwamba alikuwa na tamasha lake siku hiyo na hivyo haingewezekana.
Fat Joe ameshtakiwa na jamaa kwa jina Terrance Dixon ambaye anadai kwamba msanii huyo alijihusisha na unyanyasaji wa kikazi, kifedha , kingono na udhalilishaji.
Dixon anadai kwamba aliwahi kushuhudia Fat Joe ambaye jina lake halisi ni Joseph Cartagena, akijihusisha katika mahusiano ya kingono na watoto wa umri wa miaka 15 na 16.
Kulingana na mlalamishi, Joe alikuwa anatumia hela kushawishi watoto hao ambapo anasema katika kisa kilichohusisha binti wa miaka 16, Joe alikuwa anamlipia bili ya simu na kumnunulia mavazi, binti huyo akimlipa kwa vitendo vya kingono.
Fat Joe kupitia kwa wakili wake Joe Tacopina amekanusha madai hayo, akiyataja kuwa ya uwongo na kwamba kesi hiyo inalenga tu kumtoza pesa kwani mwasilishaji anadai fidia ya dola milioni 20.