- Katibu katika Wizara ya Usalama wa Kitaifa Dkt. Raymond Omollo anasema mashambulizi ya kigaidi yanayotokana na itikadi kali yanasalia kuwa changamoto kubwa inayolikabili taifa hili.
Ametoa mfano wa mikasa iliyopita kama vile mashambulizi yaliyotekelezwa huko Westgate, Mpeketoni, Chuo Kikuu cha Garissa na jengo la Dusit, akiongeza kuwa mashambulizi hayo yanaashiria matishio yanayolikumba taifa hili kutokana na itikadi kali za kidini.
“Matukio haya yanaashiria tishio la mara kwa mara la mashambulizi yanayochochewa na itikadi kali za kidini katika taifa letu,” amesema Dkt. Omollo.
“Matukio kama haya yanalifanya taifa letu daima kukaa chonjo.”
Dkt. Omollo aliyasema hayo leo Jumatano wakati wa uzinduzi wa “Mpango wa Kukuza Amani na Kuzuia Mashambulizi yanayotokana na Itikadi Kali Afrika Mashariki.”
Kando na itikadi kali za kidini, Dkt. Omollo alitaja mashindano ya rasilimali yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na mizozo ya mipaka kuwa chanzo kingine cha itikadi kali.