Israel imefanya mashambulizi kadhaa ya anga dhidi ya Iran mapema Jumamosi, kujibu kile jeshi lake linakiita “miezi ya mfululizo wa mashambulizi ” kutoka Tehran na washirika wake.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema kuwa linafanya “mashambulizi mahususi dhidi ya malengo ya kijeshi” nchini Iran, ambayo inaishutumu kwa “kuishambulia Israel” tangu tarehe 7 Oktoba 2023.
Uthibitisho wa IDF wa kuishambulia Iran ulifuatia ripoti za awali za vyombo vya habari vya Iran kuhusu milipuko kadhaa ndani na karibu na mji mkuu, Tehran.
Inakuja baada ya Tehran kurusha takriban makombora 200 ya balistiki kuelekea Israel tarehe 1 Oktoba, katika kile nchi hiyo ilisema ni kulipiza kisasi mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas katika ardhi ya Iran mwezi Julai.
Msemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari, alisema Israel ina “haki na wajibu” wa kujilinda na “uwezo wake wa kujihami na kushambulia” “umehamasishwa kikamilifu”.
Marekani, mojawapo ya washirika wa karibu wa Israel, ilisema shambulia la Jumamosi dhidi ya Iran ni “zoezi la kujilinda”.