Irene Ntale kutojiunga na mashirikisho ya wanamuziki

Mwimbaji huyo anasema kundi litakalomhakikishia kwamba atafaidi kwa kupata pesa ndilo atajiunga nalo.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Irene Ntale amesema kwamba hatojiunga na shirikisho lolote la wanamuziki hadi atakapohakikishiwa kwamba atanufaika kifedha.

Ntale aliyekuwa akizungumza katika mahojiano alisema yeye sio mwanachama wa chama cha wanamuziki wa Uganda – UMA na shirikisho la kitaifa la wanamuziki nchini Uganda – UNMF.

Anasema haelewi jinsi makundi hayo ya tasnia ya muziki yanaendesha shughuli zao na anashuku kwamba mazuri ya kifedha ya makundi hayo yanafurahiwa na wachache.

“Yeyote atakayeniita na kunipa sehemu ya pesa hizo ndipo nitakwenda lakini kwa sasa mimi sio mwanachama popote” Alisema Ntale akiongeza kwamba iwapo fedha husika ni za wasanii wanafaa wampigie simu kwani ana nyimbo zilizotamba na anatosha.

Msanii huyo anasema makundi hayo hupokea ufadhili lakini yanakosa kugawia wanachama kwa njia inayofaa.

“Sipingi kuwa mwanachama wa kundi fulani, lakini ninataka nifaidi pia. Mimi ni msanii stadi na kazi zangu zinajieleza” alisema Ntale.

Matamshi ya Ntale yanajiri wiki kadhaa baada ya Cindy Sanyu ambaye ni rais wa UMA kutangaza kwamba muungano wa wanamuziki wa Uganda – UMA na shirikisho la kitaifa la wanamuziki nchini Uganda UNMF zimeafikia makubaliano ya kushirikiana kwa manufaa ya wanachama wao.

Kulingana na Sanyu, vyama hivyo viwili vya kutetea maslahi ya wanamuziki vilikubaliana kushirikiana ili kuafikia lengo moja, lakini sio katika kila nyanja.

Share This Article