Irene Ntale azungumzia kuondoka kwake Swangz Avenue

Ntale aliondoka Swangz Avenue mwezi Januari mwaka 2017.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda irene Ntale kwa mara nyingine amezungumzia hatua yake ya kuondoka kwenye kampuni ya kurekodi muziki na kusimamia wasanii ya Swangz Avenue.

Akijibu maswali wakati wa mahojiano, Ntale alisema kwamba ulikuwa uamuzi wake binafsi kuondoka Swangz na alikuwa amewazia hatua hiyo kwa muda.

Ntale anasema tangu alipoondoka kwenye kampuni hiyo, amekua na ana uhuru kama mwanamuziki hata ingawa wengi wanahisi kwamba amedorora.

“Najua wengine wanasema ni kana kwamba nilipotea kwenye tasnia ya muziki tangu nilipoondoka Swangz, lakini nikitizama nyuma, nashukuru Mungu kwa uamuzi huo.” alisema Ntale.

Kati ya mambo anayojivunia ni kuweza kuunda urafiki dhabiti na wasanii wengine nchini Uganda jambo ambalo anasema halikuwezekana chini ya uangalizi mkali wa Swangz wakati huo.

Alielezea kwamba akiwa Swangz kila kitu kilikuwa kinapitia kwa meneja.

Irene Ntale alitangaza kuondoka kwake Swangz Avenue Januari mwaka 2017 kupitia akaunti yake ya Facebook na kati ya sababu alizotaja wakati huo ni kujitakia mengi zaidi kama msanii.

Kufikia sasa anasema ameafikia mengi kama msanii huru na anapata kuhisi na kuona mapato yanayotokana na sanaa yake.

Hata hivyo anashikilia kwamba Julius Kyazze, ambaye anaongoza kampuni ya Swangz Avenue ni mshauri bora hata ingawa urafiki wao ulifikia kikomo.

Wakati wa kuondoka kwa Irene kwenye Swangz Avenue, uvumi ulisambazwa mitandaoni kwamba aliondoka ghafla katika eneo la maandalizi ya video ya wimbo “Stylo”.

Hatua hiyo inaripotiwa kumghadhabisha meneja wa wakati huo ambaye sasa ni msanii kwa jina Vinka, ndiposa Irene akaamua kujiondoa.

Lakini Irene anasema huo ni uvumi tu na anahimiza mashabiki wake kuuchukulia hivyo.

Share This Article