Impala na Kabras kukabana tena katika Enterprise Cup

Martin Mwanje
2 Min Read

Kivumbi kikali kinatarajiwa kutifuka wikiendi hii katika uga wa maonyesho ya Kakamega wakati klabu za mchezo wa raga za lmpala na mabingwa mara tano na watetezi taji la Enterprise – Kabras zitakapo kabana koo tena katika raundi ya 16 ya taji la Enterprise.

Hii itakuwa mara ya pili timu hizo kuchuana msimu huu baada ya mchuano wa wikiendi iliyopita ugani mumo humo kuwania taji la Kenya cup ambapo Kabras iliiponda Impala alama 123 kwa sufuri.

Kufuatia ratiba ya jumatano hii, huenda hii ikawa fursa ya lmpala kulipiza kisasi ingawa Kabras ina makali si haba.

Katika nyuga zingine, Kenya Harlequin itamaliza udhia dhidi Catholic Monks ugani RFUEA, Menengai Oilers itachuana na MMUST uwanjani RFC Nakuru wakati Nakuru RFC ikiumiza nyasi dhidi ya South Coast Pirates ugani Nakuru Athletics Club.

Kwenye mitanange mingine, Nondescripts itawaribisha Kisumu RFC pale Ngong Racecourse huku Zetech Oaks wakisafiri hadi Strathmore Sports Complex kuzichapa dhidi ya Strathmore Leos.

KCB itawaalika wanafunzi wa chuo cha Daystar huko KCB Sports Club kisha nao wana chuo cha KU – Blak Blad wahitimishe na Mwamba RFC chuoni humo.

Robo fainali itasakatwa tarehe saba Februari ambapo washindi watachuana na timu za mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

Nusu fainali itagaragazwa tarehe 21 Machi na 11 Aprili kisha fainali ichezwe tarehe 23 mei.

Share This Article