Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), imetangaza kuwa zoezi la usajili wa wapiga kura, litarejelea mwezi Septemba mwaka huu, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon ametangaza kuwa usajili wa kitaifa wa wapiga kura utakaoanza Septemba 29, 2025 litawalenga vijana ambao wametimia umri wa miaka 18 pamoja na watu waliohitimu kupiga kura ambao hawajasajiliwa.
Hata hivyo, Ethekon alibainisha kuwa zoezi hilo litatekelezwa katika afisi za IEBC katika maeneo bunge isipokuwa maeneo ambako chaguzi ndogo zinaandaliwa.
Jumla ya chaguzi ndogo 24 zinatarajiwa kuandaliwa Novemba 27, 2025.
“Huduma zitakazotolewa ni pamoja na usajili wa wapiga kura wapya, wanaotaka kuhamia maeneo tofauti ya kupiga kura, marekebisho ya maelezo ya mpiga kura na usaili wa habari za mpiga kura,” alisema Ethekon kupitia kwa taarifa.
Kulingana na sehenu ya 83 ya Katiba ya Kenya, ili kusajiliwa kuwa mpiga kura unapaswa kuwa:
- Raia wa Kenya
- Umri wa miaka 18 na zaidi
- Kitambulisho cha taifa au Pasipoti ya Kenya
- Hajasajiliwa kuwa mpiga kura sehemu nyingine;
- Hajashtakiwa kwa makosa yanahohusiana na uchaguzi katika muda wa miaka mitano iliyopita;
- Asiye na akili taahira na
- Hajasajiliwa kwenye sajili ya wapiga kura.