IEBC mahakamani kuhusu uratibu uliochelewa wa mipaka

Tume hiyo inaitaka mahakama ya upeo itoe ushauri kuhusu iwapo mchakato huo unaweza kufanyika hata baada ya makataa ya kikatiba kuisha.

Marion Bosire
1 Min Read

Tume huru cha uchaguzi na uratibu mipaka nchini IEBC imeelekea mahakamani kutafuta ushauri wa namna ya kusonga mbele kuhusiana na mchakato uliochelewa wa uratibu mipaka.

Kuchelewa huko kulitokana na kutokuwepo kwa makamishna wa tume hiyo.

Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon ambaye aliandaa mkutano wake wa kwanza na wanahabari huko Mombasa alielezea kwamba wametafuta ushauri wa afisi ya mwanasheria mkuu kuhusu suala hilo.

Alifafanua pia kwamba wamewasilisha hoja ya kumbukumbu katika mahakama ya upeo wakitaka wapatiwe ushauri kuhusu iwapo mchakato huo wa kuratibu mipaka unaweza kutekelezwa hata baada ya kukamilika kwa muda uliowekwa na katiba.

Kuhusu mabadiliko ya sheriana udhibiti, Ethekon alisema wamewasilisha rasimu za miswada ya marekebisho na kanuni zilizorekebishwa bungeni kwa lengo la kuimarisha sheria zinazodhibiti uchaguzi.

Ethokon alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kwamba tume hiyo ya uchaguzi inapatiwa ufadhili faafu na kwa wakati ili iweze kutekeleza wajibu wake.

Kuhusu matamshi ya kisiasa kutoka kwa wanasiasa yaliyoashiria kwamba IEBC itafanya udanganyifu katika uchaguzi ili kuwapendelea, mwenyekiti huyo wa IEBC alikanusha usemi huo akiwataka viongozi wakome kuhatarisha uadilifu wa IEBC.

Share This Article