IEBC kutangaza usajili endelevu wa wapiga kura mwezi Agosti

Martin Mwanje
1 Min Read
Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon akiwa na Makamishna na Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inasema kuwa itatangaza kuanza tena kwa zoezi endelevu la uandikishaji wa wapiga kura mwezi Agosti mwaka huu. 

Vijana wengi wa kizazi cha Gen Z wameonyesha ari ya kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, kinyume cha miaka iliyopita ambapo walionekana kutokuwa na shauku ya kupiga kura.

“Naam, tunasikia sauti za vijana wanaotaka kupatiwa fursa ya kuhesabiwa na kuhusika vilivyo katika michakato ya kuijenga upya nchi yetu, Kenya,” amesema mwenyekiti mpya wa tume hiyo Erastus Edung Ethekon kwenye taarifa.

“IEBC kwa sasa inahitimisha michakato ya ndani na mwezi Agosti, 2025 itatangaza, kupitia gazeti rasmi la serikali ,muda wa kuanza tena kwa Usajili Endelevu wa Wapiga Kura (CVR) ili kuruhusu Wakenya wanaostahiki kujiandikisha kama wapiga kura.”

Matamshi yake yanakuja wakati ambapo upinzani, ukiongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, umeonya kuwa IEBC itakiona cha mtema kuni ikiwa itaonekana kukidhi maslahi ya watu binafsi katika utenda kazi wake.

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula kwa upande wake amewataka wanasiasa kukoma kuingilia kati utenda kazi wa tume hiyo na badala yake kuiacha kutekeleza majukumu yake bila kushurutishwa.

Share This Article