Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesema itashirikiana bega kwa bega na vyombo vya habari katika kuhesabu kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Hatua hiyo inalenga kuepusha hali ya mkanganyiko ambayo imeghubika shughuli ya kuhesabu kura katika chaguzi zilizopita nchini.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo Hussein Marjan, ushirikiano huo utaaidia kukabiliana na taarifa za uongo na upotoshaji na hivyo kurejesha imani ya umma katika utendaji kazi wa tume hiyo.
Kwa upande wake, mwenyekiti mpya wa IEBC Erastus Ethekon amesema tume hiyo iko tayari kuandaa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Ethekon anasema kwenye uchaguzi huo, IEBC itafanya kila iwezalo kuhakikisha hakutakuwa na vituo hewa vya kupigia kama ilivyoripotiwa awali.
Akifahamu kuwa vituo vya aina hiyo vimetumiwa siku zilizopita kushiriki udanganyifu, Ethekon anasema wamedhamiria kuziba mianya yote inayotumwa kuendeleza uovu huo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Wakati huohuo, mwenyekiti huyo amesema maandalizi ya chaguzi ndogo zitakazoandaliwa katika maeneo mbalimbali nchini yanaendelea vyema.
Ameongeza kuwa IEBC itatoa ratiba ya chaguzi hizo 24 zitakazoandaliwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Wawili hao waliyasema hayo wakati wa mkutano kati ya IEBC na mashirika ya habari uliofanyika leo Jumatano asubuhi katika hoteli moja jijini Nairobi.