Idara ya Mahakama imesitisha kimya chake na kulaani vikali idadi inayoongezeka ya visa vya ukatili wa polisi unaofanywa bila sababu za msingi humu nchini.
Aidha idara hiyo, kupitia kwa msemaji wake Paul Ndemo, imelaani hatua ya wahuni kujitokeza na kuvuruga maandamano ya amani kama ilivyoshuhudiwa jijini Nairobi jana Jumanne.
Idara ya Mahakama imevitaja visa hivyo kuwa tishio kubwa kwa utawala wa sheria nchini.
“Idara ya Mahakama inaelezea mashaka yake juu ya visa vinavyoongezeka vya ukatili wa polisi vinavyofanywa bila sababu za msingi na mwenendo unaoongezeka wa wahuni kuvuruga maandamano ya amani na kuhatarisha maisha ya waandamanaji,” alisema Ndemo kwenye taarifa leo Jumatano.
“Huduma ya Taifa ya Polisi ina jukumu la kikatiba na kisheria kutambua, kuwakamata na kuwashtaki watu kama hao pamoja na wale wanaowafadhili na kuchochea vitendo hivi vya vurugu,” aliongeza Ndemo wakati baadhi ya wanasiasa wakinyoshewa kidole cha lawama kwa kuwafadhili wahuni hao kuzua vurugu.
Idara ya Mahakama imewaelezea Wakenya kuwa itasimama kidete kuhakikisha haki inatendeka wakati ikishughulikia visa hivi, ikiwa ni pamoja na visa vilivyoripotiwa vya ukatili wa polisi.
Taarifa ya idara hiyo inakuja wakati ambapo maafisa wa polisi wameshutumiwa vikali nchini kutokana na hulka yao kandamizi inayosemekana kusababisha kifo cha mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang.
Uchunguzi kuhusu kifo hicho kilichotokea katika kituo cha polisi cha Central unaendelea na tayari Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi Eliud Lagat amejiondoa kwa muda kwenye wadhifa huo ili kuwezesha kufanywa kwa uchunguzi huru.
Maafisa wawili wa polisi pia wamekamatwa baada ya kumshambulia mchuuzi wa barakoa wakati wa maandamano ya jana Jumanne jijini Nairobi.
Mchuuzi huyo kwa jina Boniface Mwangi Kariuki anaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta, KNH ingawa ameripotiwa kuwa katika hali mahututi.
Maafisa husika wamepangiwa kufikishwa mahakamani kesho Alhamisi.
Wakenya na mashirika ya kijamii wamekuwa mstari wa mbele kulalamikia ukatili unaofanywa na maafisa wa polisi na kutoa wito kwa maafisa watundu kuwajibishwa kutokana na vitendo vyao vya kikatili.