ICC yampata na hatia ya uhalifu wa kivita kiongozi wa wanamgambo Sudan

Tom Mathinji
2 Min Read
Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman,apatikana na hatia ya uhalifu wa kivita.

Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya ICC, imempata na hatia ya uhalifu wa kivita na dhidi ya binadamu kiongozi mmoja wa wanamgambo nchini Sudan.

Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman, amaarufu Ali Kushayb, anadaiwa kutekelea makosa hayo katika eneo la Dafur alipoongoza kundi la Janjaweed ambalo linaloungwa mkono na serikali, ambapo maelfu ya watu wanadaiwa kufariki.

Kushayb anakuwa mtu wa kwanza kuhukumiwa na Mahakama ya ICC kwa ukatili uliotekelezwa Darfur.

Majaji walimpata na hatia ya mauaji ya halaiki, dhuluma za kimapenzi na mateso wakati wa mashambulizi yaliyotekelezwa baina ya mwaka 2003 na 2004. Kushayb alikanusha mashtaka hayo akisema yalitekelezwa na mtu mwingine ila manusura walitoa ushahidi kwamba aliongoza mashambulizi dhidi ya jamii zao.

Mzozo huko Darfur ulioanza mwaka 2003, umesababisha vifo vya takriban watu laki-3 huku mamilioni ya wengine wakipoteza makazi.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yamepongeza uamuzi wa kumpata na hatia wakisema ni hatua ya kihistoria katika kupata haki ingawa ripoti za ghasia zinazoendelea na utocu wa usalama zimeendelea kuchipuza kutoka kwenye eneo hilo.

Janjaweed waliwashambulia wanakijiji wasiokuwa Waarabu wanaoshutumiwa kuwaunga mkono waasi, na kusababisha shutuma za mauaji ya halaiki.

Wengi wa wapiganaji wa Janjaweed wamejiingiza na RSF, kikundi cha wanamgambo ambacho kwa sasa kinapambana na jeshi la Sudan.

Uingereza, Marekani na mashirika ya kutetea haki za binadamu yameishutumu RSF kwa kutekeleza mauaji ya kikabila dhidi ya jamii zisizo za Kiarabu huko Darfur tangu mzozo huo uanze mwaka 2023.

Share This Article