Ibraah ashukuru waliorejesha tabasamu ya mamake

Hii ni baada ya kupokea michango ya kifedha kutoka kwa mashabiki pesa ambazo alitumia kulipia matibabu ya mamake.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Ibraah ameshukuru mashabiki wake wa Tanzania na wa nchi nyingine kutokana na kile alichokitaja kuwa hatua yao ya kurejeshea mamake mzazi tabasamu.

“Asanteni sana watanzania wenzangu ambao mmenichangia leo. Kila alipo aliyenichangia amenisaidia kurudisha tabasamu la mama yangu mzazi.” aliandika Ibraah kwenye akaunti yake ya Instagram.

Huku akichapisha picha ya maelezo ya kumtumia pesa, Ibraah aliwaombea wote waliomchangia baraka kutoka kwa mwenyezi Mungu.

Anasema hata ingawa hataweza kumudu kulipa shilingi Bilioni moja anazodaiwa na kampuni ya Konde Music kabla ya kuvunja mkataba nao, anafurahia mamake amenusuriwa.

Siku chache zilizopita, mwanamuziki huyo aliomba usaidizi wa kifedha kwa umma akisema kwamba alihitajika kupata pesa za kulipa kampuni hiyo inayomilikiwa na Harmonize ila hakusema kwamba mamake anaugua.

Ameelezea kwamba mamake amelia baada ya kufahamishwa zilikotoka pesa za kugharamia matibabu yake huku akiwashukuru.

Wakati huo huo msanii huyo amezomea wale ambao wanadhania ombi lake ni mzaha akisema, “Na kwa wale wanaowaambia ni kiki basi kwenye ufalme wa Mungu wakapuuzwe wakiwa katika fungu la waonevu.

Kufikia sasa kampuni ya Konde Music haijatoa taarifa rasmi kuhusu madai ya Ibraah ya kutakiwa kulipa bilioni moja kabla ya kuondoka humo.

Share This Article