Hukumu ya kifo ya Nduta yabatilishwa hadi kifungo cha maisha

Tom Mathinji
1 Min Read
Margaret Nduta aliyekuwa amehukumiwa kifo Vietnam, sasa atatumika kifungo cha maisha.

Serikali imetoa wito kwa Wakenya wanaoishi, kufanyakazi au wanaosafiri ng’ambo, kuheshimu sheria za nchi husika, ili kuepuka kujipata pabaya.

Wito huo unajiri kufuatia ufanisi wa kidiplomasia ambapo Mahakama ya Juu nchini Vietnam imebatilishi hukumu ya kifo ya Margaret Nduta hadi kifungo cha maisha. Tangazo hilo lilitolewa na katibu  wa maswala ya Ughaibuni Roseline Njogu, aliyesisitiza haja ya kuheshimu sheria ughaibuni.

“Tunawakumbusha raia wote wa Kenya wanaosafiri ng’ambo kuheshimu na kuzingatia sheria za nchi wanako kwenda na kujiepusha na shughuli haramu zitakazowasababisha kukiuka sheria,” alisema Katibu Njogu.

Awali Nduta, aliyekuwa amehukumiwa kifo, alipata afueni wakati wa kikao cha mahakama wiki hii. Katibu Njogu alihusisha ufanisi huo na mashauriano ya kidiplomasia kati ya serikali ya Kenya na utawala wa Vietnam.

Pia alishukuru ubalozi wa Kenya Jijini Bangkok, Thailand, kwa msaada wake wa kisheria na kuwashukuru wanachama wa ughaubuni walio katika eneo la ASEAN waliohudhuria kikao hicho cha mahakama kuonyesha umoja wao.

Huu ni ufanisi wa pili wa kidiplomasia katika siku za hivi karibuni, baada ya Kenya kuingilia kati na kuwezesha kuachiliwa huru kwa Stephen Munyakho aliyekuwa amehukumiwa kifo Arabia.

Share This Article