Tanzania ilipata tiketi ya robo fainali ya makala ya nane ya kipute cha Afrika kwa wanandinga wa ligi za nyumbani CHAN, baada ya kuwashinda Madagascar magoli 2-1, jana jioni uwanjani Benjamin Mkapa.
Mchuano huo wa kundi B ulishuhudia mshambulizi Clement Mzize, akipachika mabao mawili dakika ya 13 na 20 huku Mika Razafimahatana, akikomboa moja kwa wageni dakika ya 34.
Taifa Stars wamedumisha rekodi ya asilimia 100 wakiongoza kwa pointi 9, wakifuatwa na Mauritania kwa alama 4 huku Burkina Faso ikiwa na alama 3.
Aidha, Tanzania wamo mbioni kuongoza kundi hilo, hali itakayowapa fursa ya kuandaa mchuano wa kwanza wa robo fainali katika uwanja wa Benjamin Mkapa.
Awali katika uwanja wa Mkapa, Mauritania waliibwaga Jamhuri ya Afrika ya Kati bao moja bila jawabu.