Hospitali za kibinafsi zatoa ilani ya mgomo ya siku 14

Tom Mathinji
2 Min Read

Chama cha hospitali za kibinafsi (RUPHA), kimetoa ilani ya mgomo ya siku 14 kwa Halmashauri ya Afya ya Jamii  (SHA), kikitaja hatua ya serikali kukosa kutoa malipo ya SHA yanayodaiwa na hospitali hizo.

Mwenyekiti wa RUPHA  Brian Lishega, alisema hospitali za kibinafsi zinakabiliwa na changamoto, huku zikiidai serikali ya taifa kitita cha shilingi bilioni 76.

Kupitia kwa taarifa, Lishenga alisema deni hilo linadumaza utoaji huduma, kutokana na ukosefu wa dawa, wafanyakazi na fedha za kuendesha shughuli.

“Hospitali za hapa nchini zinakumbwa na changamoto kuu ya kifedha kutokana na serikali kukosa kulipa malimbikizi ya SHA,” alisema Lishenga kwenye taarifa hiyo.

Lishenga alisema asilimia 50 ya deni kwenye hospitali za level 2 hadi level 4 halijalipwa, na kusababisha tatizo kubwa la kifedha kwenye hospitali hizo.

Wakati huo huo, Lishega aliinyoshea kidole cha lawama Halmashauri ya SHA kwa kukaidi agizo la Rais lililotolewa Machi 5,2025 la kulipwa kwa deni lililodaiwa iliyoyokuwa Hazina ya Bima ya Afya NHIF.

Kulingana naye deni la NHIF ni shilingi bilioni 33, huku deni la SHA likiwa shilingi bilioni 43, deni jumla likiwa shilingi bilioni 76.

Ili kushughulikia tatizo hilo, RUPHA inapendekeza kulipwa kikamilifu kwa deni linalodaiwa NHIF, malipo ya angalau asilimia 50 ya shilingi bilioni 43 kutoka kwa SHA, kubuniwa kwa mkakati wa kudhibitisha malipo ya SH, kubuniwa kwa jopo la kushughulikia uchapishaji kwa njia ya uwazi deta kuhusu malipo.

“Bila kuchukuliwa hatua za dharura, mfumo wa afya nchini utasambaratika,” alionya Lishenga.

Share This Article