Hospitali ya Chiromo yafungwa kufuatia kifo tatanishi cha Susan Njoki

Tom Mathinji
2 Min Read
Susan Njoki alifariki kwa njia tatanishi katika hospitali ya Chiromo.

Chama cha Madaktari, Wataalam wa Dawa na Meno hapa nchini  (KMPDC), kimeanzisha uchunguzi kuhusiana na madai ya mauaji ya Susan Kamengere Njoki, ambaye alikuwa muuguzi na mwanzilishi wa shirika la Toto Touch.

Hatua hii inafuatia uchunguzi wa maiti uliofanyiwa mwili wa Njoki Jumanne Julai 22, 2025 uliobainisha kuwa alifariki baada ya kulazimishwa kulazwa kwenye hospitali ya Chiromo, huku matokeo yakiashiria kuwa alinyongwa.

Kufuatia kisa hicho, hospitali hiyo imeagizwa kusitisha shughuli zake na kuwaondoa wagonjwa wote mara moja, kutoa fursa kwa uchunguzi.

“Baraza hili linafahamisha umma kwamba limeanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha marehemu Susan Kamengere Njoki, aliyefariki akipokea matibabu katika hospitali ya Chiromo,” kilisema chama hicho kupitia kwa taarifa.

“Kuambatana na uchunguzi unaoendeshwa na chama hichi na asasi zingine, tawi hilo limeagizwa kuwahamisha wagonjwa wote ili kutoa fursa kwa uchunguzi,” iliongeza taarifa hiyo.

Njoki, ambaye amekuwa akipokea matibabu ya matatizo ya akili, aliandika kwenye mitandao yake ya kijamii kwamba mume wake Alloise Ngure, aliwatuma watu wanne kumchukua nyumbani kwake Kileleshwa na kumpeleka hospitalini bila mapenzi yake.

Ngure, alikamatwa na maafisa wa polisi na baadaye kuachiliwa kwa dhamana baada ya kuandikisha taarifa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali hiyo Dkt. Vincent Hongo, siku ya Jumanne alisema wanashirikiana kwa karibu na maafisa katika uchunguzi wa kifo hicho.

Uchunguzi wa awali umebainisha kuwa, kifo cha Njoki kinahusiana na hali yake ya afya.

Share This Article