Henry Mayanja asimulia kuhusu mambo angependa kumwambia Rais

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Henry Mayanja, amefichua mambo ambayo angeyapa kipaumbele iwapo angepata fursa ya kukutana na Rais Yoweri Museveni kujadili masuala yanayoathiri tasnia ya sanaa na burudani.

Mayanja anahisi kwamba kwanza, kunafaa kuanzishwa kituo cha redio na runinga vya serikali, ambavyo vitajitolea kikamilifu kuendeleza kazi za ubunifu, hata kabla ya wasanii kushinikiza marekebisho na kupitishwa kwa sheria ya hakimiliki.

Mwimbaji huyo anadai kwamba wasanii hawafai, kwa sasa, kudai ulinzi wa hakimiliki ilhali tasnia haina majukwaa yake makubwa ya vyombo vya habari ya kukuza maudhui ya ndani.

Amesisitiza kwamba redio na televisheni bado ndiyo njia za kuaminika zaidi za kutangaza muziki na zitabaki kuwa muhimu kwa miongo kadhaa ijayo.

Mayanja pia alieleza wasiwasi kwamba mara tu sheria ya hakimiliki itakapopitishwa, wanamuziki wengi wa Uganda wanaweza kukabiliwa na mashtaka, hususan kutoka kwa wanamuziki wa Nigeria, kwa sababu baadhi yao wametumia dhana za muziki kutoka Nigeria bila kupata ruhusa.

“Wakati sheria ya hakimiliki itakapopitishwa, wanamuziki wetu wengi huenda wakashtakiwa na Wanaigeria kwa sababu wasanii wengi hapa wametumia maudhui yao bila ruhusa.” Alisema.

Suala la hakimiliki limekuwa donda sugu kwa wabunifu nchini Uganda na katika kongamano kuhusu hakimiliki jijini Kampala mwezi septemba mwaka huu, wadau walihimiza utekelezaji wa sheria ya hakimiliki.

Kongamano hilola “African Regional Seminar on Copyright and Related Rights” liliandaliwa Septemba 10 na 11, 2025 na serikali ya Uganda, shirika la Afrika kuhusu mali ya kiakili na mashirika mengine.

Share This Article