Hengdian: Mji wa China unaofahamika kama ‘Chinawood’ unaovutia watalii kila uchao

Martin Mwanje
3 Min Read
Hengdian World Studios zinazopatikana mjini Hengdian, China

Katika jiji la Dongyang katika mkoa wa Zhejiang, kusini mashariki mwa China, unapatikana mji wa Hengdian.

Awali, wakazi wengi waliuhama mji huo kwenda kutafuta kazi kwingineko kwa sababu haukuwa umepiga hatua kubwa kimaendeleo.

Lakini miaka michache baaaye, Hengdian sasa umeibuka kuwa mji uliopiga hatua kubwa kimaendeleo, wenye vivutio vingi vya kitalii, na unaofahamika sana kama kitovu cha uigizaji nchini China.

 

 

Maendeleo hayo yamewafanya wengi sasa kuanza kumiminika mjini humo ama kutafuta ajira au kujiburudisha kwa jinsi ulivyobobea kutokana na michezo ya kuigiza.

Isitoshe, mji wa Hengdian unaofahamika kama “Chinawood” ni makazi ya Studio za Hengdian Duniani, maarufu kama “Hengdian World Studios.”

Katika studio hizo, teknolojia za kisasa zinazofahamika sana kama “virtual technology”, miongoni mwa zingine, zinatumika kurahisisha utayarishaji wa filamu kwa kupunguza gharama na muda wa kutengeneza filamu hizo.

Nazo studio hizo zimetekeleza jukumu kubwa katika kuzalisha waigizaji mahiri ambao wameigiza katika filamu za Kichina na ambazo zimejizolea sifa tele kote duniani.

Lakini hizo si studio pekee za kutengeneza filamu katika mji wa Hengdian.

Kila uendako, utabaini uwepo wa kampuni nyingi zinazotengeneza filamu na kukuza vipaji vya vijana wengi waliozamia tasnia ya uigizaji.

Wakati ukitembelea maeneo mengi ya mji huo yaliyotengwa kutambulisha ama utamaduni wa China kwa dunia au kutumiwa kwa ajili ya uigizaji, utakumbana na shughuli nyingi za kurekodi tamthilia, zingine fupifupi, zikiendelea.

Nje ya malango ya kampuni nyingi za kutengeneza filamu, raia wengi wa China nao hujitokeza na kuvuta subira, wakiwa na shauku ya kuwaona waigizaji maarufu ambao wamekonga nyoyo zao kupitia kazi zao za uigizaji.

 

Kwa upande mwingine, kumbi mbalimbali za mji huo hufurika raia wengi wa China na wale wa kigeni wanaofika kujionea tamthilia zinazoangazia mada mbalimbali.

 

 

Ni tamthilia zilizosukwa na kuigizwa kwa ustadi mkubwa ili kukidhi mahitaji ya hadhira, mahitaji ambayo kufikia mwishoni mwa tamthilia hutimizwa na kuwaacha wengi wakitawaliwa na tabasamu.

“Ilipendeza lakini ilikuwa na sehemu zilizotia hofu. Nilihofia baadhi ya waigizaji wangeanguka,” alisema mwanamke mmoja kutoka Uholanzi baada ya kutazama mchezo mmoja wa kuigiza.

 

 

Katika baadhi ya maeneo, kama vile Makazi Mapya ya Hengdian New Yuanmingyuan, maisha ya mfalme yamesawiriwa kupitia majengo yaliyojengwa eneo kubwa zaidi na kugharimu mamilioni ya yuan.

“Ujenzi wa eneo hili uligharimu takriban yuan milioni 30,” alisema mwongozaji wangu wakati akinionyesha mahali alipokuwa akilala mfalme zama zile.

 

 

Kwenye barabara za mji wa Hengdian, utakumbana na mabasi kila baada ya sekunde yaliyowabeba watalii kutoka kila sehemu ya dunia, waliokuja kujionea maendeleo ya kasi ya “Chinawood”.

Hadi kufikia wakati wakiondoka, wao husikika wakiungama namna hakika mji wa Hengdian ulivyopania kuwa kitovu cha uigizaji duniani, yawezekana ukilenga kupiku “Hollywood.”

 

 

TAGGED:
Share This Article