Tume Huru ya Kuangazia Utenda Kazi wa Polisi (IPOA) sasa inasema haina uwezo wa kuchunguza visa vya utekaji nyara humu nchini.
Matamshi ya IPOA yanakuja wakati ambapo kumekuwa na ongezeko la visa vya utekaji nyara vinavyodaiwa kutekelezwa na maafisa wa polisi.
Mwenyekiti wa tume hiyo Issack Hassan anasema ingawa baadhi ya Wakenya wanaamini kuwa utekaji huo unafanywa na polisi, Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja amekanusha madai hayo.
Kwa misingi hiyo, Hassan amesema IPOA haiwezi ikachunguza visa hivyo hadi polisi wakiri kuwa wanahusika katika utekaji huo.
Ametaja uhaba wa maafisa wa upelelezi kuwa changamoto katika kuchunguza visa vinavyoongezeka vya utekaji nyara nchini, ikizingatiwa kuwa tume yake ina maafisa 77 pekee wa upelelezi.
Hassan aliyasema hayo wakati akiwahutubia wanahabari mjini Meru alipoongoza makamishna wapya wa IPOA katika kutembelea ofisi ya kanda hiyo kujifahamisha juu ya utenda kazi wake.
Taasisi mbalimbali ikiwemo Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu (KNCHR) na Chama cha Wanasheria nchini (LSK) zimekuwa katika mstari wa mbele kulaani kushamiri kwa visa vya utekaji nyara nchini na kutoa wito kwa serikali kuhakikisha vinakomeshwa mara moja.
Isitoshe, Kanja na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin wameshtakiwa kuhusiana na utekaji huo.
Taarifa hii imechangiwa na Jeff Mwangi