Mataifa hasa yanayoendelea kote duniani yameanza kuhisi athari za utawala mpya wa Marekani unaongozwa na Rais Donald Trump.
Tangu alipoingia madarakani Januari 20, Trump ametia saini amri za rais zaidi ya 20 zinazokusudia kuirejeshea Marekani hadhi yake ya zamani duniani na kulainisha mambo kadha wa kadha ambayo utawala huo unahisi yalikuwa yameenda mrama.
Miongoni mwa amri hizo ni ile inayolenga kuiondoa Marekani kutoka kwenye Shirika la Afya Duniani, WHO.
Aidha, Rais Trump ametangaza kusitishwa kwa msaada wa kigeni ambao husaidia katika kukabiliana na maradhi kama vile Ukimwi na kifua kikuu, na ambao kwa kawaida hutolewa kupitia shirika la USAID.
“Tangazo la hivi karibuni la Marekani kujiondoa WHO na kusitisha msaada wa kigeni, ikiwa ni pamoja na mipango muhimu kama vile Mpango wa Dharura ya Rais kwa ajili ya Msaada wa Ukimwi (PEFAR) unaashiria kuanza kwa wakati muhimu wenye athari kubwa kwa mataifa kote duniani, ikiwemo Kenya,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Patrick Amoth wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumatano.
“Kenya imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya Ukimwi, kwa kiwango kikubwa ikisaidiwa na mipango ya dunia kama vile PEFAR.”
Kulingana na Dkt. Amoth, kati ya watu milioni 1,377,784 wanaoishi na virusi vya Ukimwi, watu milioni 1,352,657 wanafahamu hali zao na wamepimwa na wanapatiwa matibabu huku watu milioni 1,299,330 wanaotibiwa wakifanikiwa kuvikandamiza virusi vya ugonjwa huo.
Amesema ushirikiano kati ya Kenya na Marekani umefanikiwa kufikia malengo yake katika kukabiliana na changamoto katika sekta ya afya nchini.
“Ushirikiano huu umetekeleza wajibu muhimu katika kuimarisha mifumo ya afya nchini Kenya kupitia mipango ya ushirikiano, mipango ya ukuzaji uwezo, na msaada wa rasilimali, na kuchangia kwa kiwango kikubwa kwa mafanikio katika nyanja kama vile kuzuia magonjwa, mipango ya matibabu, na maendeleo ya miundombinu ya afya,” aliongeza Dkt. Amoth.
Kufuatia hatua ya Marekani, Mkurugenzi huyo, miongoni mwa mambo mengine, ameelezea hofu kuwa utoaji matibabu kwa wagonjwa wa Ukimwi huenda ukatatizika na uambukizaji wa maradhi hayo kutoka kwa mama hadi kwa mtoto kuongezeka.
Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa ameashiria kuwa Kenya huenda ikalazimika kutafuta ufadhili mbadala kutokana na hatua iliyochukuliwa na serikali ya Marekani.