Timu ya taifa Harambee Stars imesajili ushindi wa kihistoria wa bao moja kwa bila dhidi ya miamba Morocco katika mchuano wa kundi A kuwania kombe la CHAN uliosakatwa uwanjani Kasarani.
Kenya walipata bao pekee na la ushindi kupitia kwa Ryan Ogam kunako dakika ya 42 ya mchezo.
Licha ya kiungo Erastus Erambo, kupigwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza, Kenya walijihami hadi wakapata ushindi.
Harambee Stars wanaongoza kundi A kwa alama 7, baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare moja.
Kenya itarejea uwanjani Kasarani kwa mchuano wa mwisho dhidi ya Zambia Jumapili ijayo.