Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars, imeripoti kambini leo Alhamisi kujiandaa kwa makala ya nane ya michuano ya Kombe la Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani, almaarufu CHAN.
Waziri wa Michezo Salim Mvurya ametoa changamoto kwa timu hiyo kutumia uwanja wa nyumbani na kusajili matokeo bora.
Mvurya alisema hayo siku ya Alhamisi aliposhuhudia kikosi hicho kikiripoti kambini rasmi.
Kenya imejumuishwa kundi A pamoja na DR Congo walionyakua mataji mawili, Morocco ambao pia ni mabingwa mara mbili, Angola na Zambia.
Kipute cha CHAN kimeratibiwa kuandaliwa kati ya tarehe 2 na 30 mwezi ujao katika mataifa ya Kenya, Uganda na Tanzania.