Timu ya taifa ya soka Harambee Stars imeendeleza mazoezi kujiandaa kwa mechi ya robo fainali kuwania kombe la CHAN dhidi ya Madagascar, Ijumaa hii katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.
Stars waliomaliza wa kwanza kundini A kwa pointi 10 baada ya kushinda mechi tatu na kwenda sare moja,wakifunga mabao 4 na kufungwa moja.
Upande wao Madagascar walimaliza katika nafasi pili kundini B kwa alama 7,wakishinda mechi mbili kushindwa moja na kwenda sare moja wakifunga magoli matano na kufungwa matatu.
Ni mara ya kwanza kwa Kenya kufuzu kwa kipute cha CHAN huku Madagascar, wakiwania kutwaa kombe la kwanza baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu mwaka 2022 nchini Algeria.
Mechi hiyo itang’oa nanga saa kumi na moja jioni.
Mshindi wa robo fainali ya Kenya na Madagascar atamenyana na mshindi wa kwota fainali ya mwisho kati ya Algeria na Sudan.